AfCFTA: Ndoto za kijana mfanyabiashara zatimia

Get monthly
e-newsletter

AfCFTA: Ndoto za kijana mfanyabiashara zatimia

Mjasiriamali Mkenya wa miaka thelathini, Linda Chepkwony anataka kuwahamasiha vijana wa Kiafrika kusaidia kukuza viwanda barani kupitia mkataba wa biashara huria
Kingsley Ighobor
Afrika Upya: 
9 February 2023
Linda Chepkwony Linda is shifting her business model to adding value to commodities such as honey an
Linda Chepkwony is adding value to commodities such as honey and nuts and then exporting them to other African countries.

Linda Chepkwony analenga macho yake angani. Ana ndoto ya kuwa bilionea wa kwanza kijana barani Afrika. Anataka pia kusaidia mageuzi ya hali ya kiuchumi ya bara hili

​Safari ya ujasiriamali ya Mkenya huyu mwenye umri wa miaka 30 ilianza kwa kusafirisha bidhaa za sanaa na ufundi Marekani, bila kutozwa ushuru chini ya (African Growth and Opportunity Act) Sheria ya Ukuaji na Fursa Afrika - ambayo hutoa ufikiaji wa soko la Marekani bila kutozwa ushuru kwa bidhaa teule kutoka mataifa fulani ya Afrika.

Hata hivyo, huku Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) likianza kutumika, Linda anabadilisha mtindo wake wa biashara kwenye kuongeza thamani ya bidhaa kama vile asali na karangana kisha kuzisafirisha katika mataifa mengine ya Afrika.

AfCFTA ina uwezekano wa kuunganisha soko la bilioni 1.3 na Pato la Taifa la dola trilioni 3.4, kuondoa ushuru wa bidhaa na huduma nyingi, na kuhakikisha usafirii huria wa nguvumali miongoni mwa mataifa yanayoshiriki.

AfCFTA itarahisisha na kuharakisha biashara, sio kwangu tu bali kwa mamilioni ya wanawake na vijana barani Afrika. Itakuwa ya ajabu!

Mkataba huo wa kibiashara unaonekana kutayarishwa kwa ajili ya Linda: yeye ni mchanga, mjasiriamali, mwanamke, na mtaalamu wa teknolojia. Ana ndoto ya Afrika ambayo imekombolewa kutoka kwa minyororo ya maendeleo duni. Anaamini vijana wanaweza kuongoza hatua. Na ana roho ya ‘naweza kufanya’ pamoja na hisia ya udharura.

Uongezaji thamani

Linda ni mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya RiftValley Organics Africa yenye makao yake makuu nchini Kenya – kampuni ambayo inasindika na kufungasha asali, karanga, siagi ya njugu na bidhaa za mitishamba na mbegu kwa ajili ya soko la ndani, pamoja na masoko mengine ya Afrika.

Hivi sasa, anajishughulisha na uongezaji thamani.

Bidhaa zake maarufu ni pamoja na chai iliyotiwa mchaichai-ndimu, minti, ndimu, tangawizi au mdalasini. Pia kuna asali iliyotiwa tangawizi na siagi ya karanga yenye krimu.

Linda anapata bidhaa ghafi zaidi ndani ya nchi, ingawa wakati mwingine anaagiza kutoka mataifa jirani.

"Wakati mwingine, kuna msimu wa uhaba wa asali nchini Kenya na utashi ni mkubwa, hivyo ninapata asali kutoka Tanzania au Uganda ili kukidhi upungufu," anasema.

Changamoto, hata hivyo, ni kwamba wakati mwingine kile kinachopatikana katika mataifa haya sio cha ubora unaofaa. "Kwa mfano, karanga zinaweza kuwa na aflatoxin [fangasi fulani]. Hiyo ina maana kwamba hatutahitajika kuzishughulikia.”

Kuna fursa nyingi za soko barani Afrika. Mengi ya mataifa yetu huagiza bidhaa za kilimo kutoka Magharibi, ilhali bidhaa hizo zinapatikana kwa urahisi barani Afrika.

Tofauti na mikataba ya kitamaduni ya kibiashara ambayo inazingatia biashara ya bidhaa, huduma, na haki miliki, kimawazo, AfCFTA ina lengo pana zaidi linalojumuisha kuwajumuisha vijana na wanawake katika juhudi za kukuza viwanda barani Afrika. Tangu awali, viongozi wa Afrika walidai itifaki juu ya wanawake na wafanyabiashara vijana.

Wamkele Mene, Katibu Mkuu wa Afisi ya AfCFTA, aliiambia Afrika Upya katika (interview) mahojiano ya awali kwamba “Sababu ya kuangazia zaidi vijana wa Kiafrika na SMEs (biashara ndogo na za zinzoinuka) zinazoongozwa na wanawake ni kwamba, kwanza, wao ndio vichochezi vya uchumi wa Afrika. SMEs zinazoendeshwa na wanawake zinachangia karibu asilimia 60 ya Pato la Kitaifa la Afrika, na kubuni ajira zipatazo milioni 450.”

Linda anazungumza kuhusu "kutumia uwezo wa vijana katika Afrika katika kuongeza thamani" na anasisitiza kwamba "lazima Afrika ijilishe yenyewe."

Kwa hivyo, anatumai "kuwa na vituo vya utengenezaji na uvumbuzi katika mataifa tofauti ya Kiafrika ambapo vijana wanaweza kujifunza kuhusu teknolojia ya utengenezaji, kuhusu uongezaji wa thamani ili waweze kuwa na bidhaa zinazofaa kwa soko linalofaa."

Biashara chini ya AfCFTA ilianza rasmi Januari 2021, na, licha ya changamoto za awali, Linda anahisi kuwa bara hili liko kwenye kilele cha mageuzi ya kibiashara.

"AfCFTA itarahisisha na kuharakisha biashara, sio kwangu tu bali kwa mamilioni ya wanawake na vijana barani Afrika. Itakuwa ya ajabu!” anasema.

Cheti cha Kanuni za Asili

Hivi majuzi, Linda alipokea Cheti cha Kanuni za Asili, ambacho kinapunguza ushuru wa bidhaa zake kutoka asilimia 35 hadi 24.5.

Kanuni za Asili za AfCFTA zimeweka miongozo ya mapendeleo ya ushuru kwa bidhaa zinazokidhi kanuni za asili na zinazouzwa ndani ya eneo la biashara huria.

Linda Chepkwony
Linda Chepkwony
Jinsi nilivyopata cheti changu cha biashara cha Kanuni za Asili katika siku moja

Kenya imerahisisha sana utoaji wa cheti cha Kanuni za Asili. Nilikipata changu kwa siku moja tu.

Cheti cha Kanuni za Asili ni muhimu kwa sababu kinaonyesha kuwa bidhaa zangu zinatoka Kenya na kwa hivyo zinahitimu upendeleo wa ushuru, au ushuru wa bei nafuu wa kuagiza, ndani ya mataifa ya Eneo la Biashara Huria za Bara la Afrika.

Nchini Kenya, Idara ya Forodha na Udhibiti wa Mipaka iko chini ya Mamlaka ya Mapato ya Kenya (Kenya Revenue Authority)  (KRA). Ili kurahisisha kutuma maombi ya Cheti cha Kanuni za Asili, KRA imeanzisha afisi katika kaunti tano (Nairobi, Mombasa, Nakuru, Uasin Gishu na Kisumu) kote nchini. Hata usipokuwa katika jiji kuu, Nairobi, unaweza kutuma maombi ya cheti katika kaunti yoyote kati ya hizo.

Kwa upande wangu, nilienda ofisini Nairobi. Niliwaambia maafisa wa pale kuwa nilifika kuomba cheti cha Kanuni za Asili.

Walikagua ushuru wa bidhaa zangu. Kwa sababu tunafanya biashara ya karanga na asali, kiwango chetu cha ushuru kilikuwa asilimia 35. Walinifahamisha kuwa ushuru wa bidhaa zangu utakuwa asilimia 24.5 ikiwa nitapata cheti. AfCFTA inaeleza kuwa viwango vya ushuru kwa bidhaa nyingi hushuka hatua kwa hatua hadi kufikia mwaka 2030 utakapoondolewa kabisa.

Maafisa hao walinipa fomu ya maombi ambamo nilitaja bidhaa zangu na nchi zinakopelekwa.

Kwa hivyo, mara nilipojaza fomu, waliangalia katika mfumo wa msimbo wa HS [Harmonized System] wa bidhaa zangu. Msimbo huo umeonyeshwa kwenye cheti cha Kanuni za Asili. Kila bidhaa ina msimbo wa kipekee wa HS.

Lazima niseme kwamba nilipokea, mapema, baadhi ya hati kutoka kwa washirika wangu nchini Ghana, ikiwa ni pamoja na ankara. Kiasi cha bidhaa zinazosafirishwa hadi mataifa mengine ziko kwenye cheti cha Kanuni za Asili ili kusaidia maafisa wa forodha nchini Ghana katika taratibu za kupokea na kukagua bidhaa.

Baada ya hapo, nililipa kiwango sawa na $3. Kisha maafisa wa KRA walipanga ukaguzi wa vifaa vyetu vya uzalishaji pamoja na bidhaa. Walifanya hivi ili kuthibitisha kwamba tunapata malighafi na kumaliza utengenezaji bidhaa nchini Kenya.

Maafisa hao walichukua sampuli za bidhaa zetu kwa uchunguzi wa kina. Mara tu baada ya kuthibitishwa na kulipa ada ya $ 3, nilipewa cheti cha Kanuni za Asili cha AfCFTA pamoja na barua ya usajili kama msafirishaji nje wa AfCFTA.

Mataifa yanayohusika katika AfCFTA yanajitolea kupunguza hadi asilimia 90 ya ushuru wa forodha kwa biashara ya bidhaa na huduma ifikapo mwaka wa 2030. Kwa hiyo, Linda anatarajia kupunguzwa zaidi kwa ushuru wa bidhaa zake ifikapo mwaka ujao, kupunguzwa tena 2025, na kuendelea.

Ametumia kwa hamu fursa ya Mpango wa Biashara Elekezi (Guided Trade Initiative) kusafirisha shehena ya asali iliyotiwa mitishamba kutoka Kenya hadi Ghana. Alikutana na washirika wake Waghana na wengine kupitia fursa zinazotolewa na Tume ya Kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) Afrika kushiriki katika matukio mbalimbali ya kibiashara barani humu.

Mpango wa Biashara Elekezi unaruhusu biashara ya baadhi ya bidhaa kati ya mataifa manane (Kameroon, Misri, Ghana, Kenya, Mauritius, Rwanda, Tanzania na Tunisia) ambazo zinakidhi vigezo fulani, ikiwa ni pamoja na kufuata maelekezo ya Kitabu cha Ushuru cha AfCFTA na Mwongozo wa Kanuni za Asili na uchapishaji wa viwango vya ushuru vilivyoidhinishwa na afisi ya AfCFTA.

"Baada ya Ghana, ninalenga Kameroon na kisha Misri kwa chai yetu iliyotiwa mitishamba," anasema Linda.

Anakusudia kushirikiana na vijana wenzake kuanzisha vituo vya uzalishaji katika mataifa mengine. Anauita mkakati huo "fursa za kuungana."

Anafafanua: “Kama taifa lina malighafi ambayo tunaweza kuiongezea thamani, tuseme korosho katika Ivory Coast, tutawawezesha vijana wa huko kufanya uongezaji thamani katika korosho —unga wa korosho, siagi ya korosho, korosho ya chokoleti na korosho ya kuchoma.

"Itarahisisha kazi yetu. Tutatimiza maagizo katika soko hilo bila vizuizi vyote vya taaratibu za usafirishaji wa bidhaa kutoka Kenya hadi taifa hilo. Na tutatengeneza ajira ambazo zitawasaidia vijana kuboresha maisha yao.”

Anasisitiza “Kuna fursa nyingi za soko barani Afrika. Mengi ya mataifa yetu yanaagiza bidhaa za kilimo kutoka Magharibi, ilhali bidhaa hizo zinapatikana kwa urahisi barani Afrika.”

Changamoto

Licha ya matamanio yake makuu, Linda anaelewa matatizo ya sasa yanayowakabili wajasiriamali wadogo.

Kwanza ni ukosefu wa upatikanaji wa mtaji.

"Ni vigumu kwa vijana kupata mitaji katika viwanda na sekta nyinginezo. Mfanyabiashara kijana anaanza kwa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu biashara, kukokotoa gharama za uzalishaji, kulinganisha alama na faida, lakini watakata tamaa kirahisi bila mtaji wa kuanzia,” anasema.

Ikiwa taifa lina malighafi ambayo tunaweza kuongeza thamani yake, tuseme korosho ya Ivory Coast, tutawawezesha vijana wa huko kufanya uongezaji thamani katika korosho—unga wa korosho, siagi ya korosho, korosho ya chokoleti na korosho za kuchoma. Itarahisisha kazi yetu. Tutatimiza maagizo katika soko hilo bila vizuizi vyote vya taratibu za usafirishaji… na tutaunda nafasi za ajira ambazo zitawasaidia vijana kuboresha maisha yao.

Pili, ugumu katika harakati za kuvuka mpaka ni changamoto pia.

Anakumbuka: “Hivi majuzi, nilikuwa nikitazama Mwana-YouTube ambaye alisema alikuwa na matatizo ya kutoka Togo hadi nchini mwake, Ghana, kwamba aliombwa mpakani alipe fedha fulani.

"Ikiwa kwenda katika nchi yako kupitia kituo cha mpaka cha jirani kuna changamoto, unawezaje hata kufanya biashara?" anahoji.

Tatu, kuna changamoto za utaratibu wa usafirishaji zinazokabili SMEs barani Afrika.

“Unaombwa kutoa rundo la hati mpakani. Mtu hata huumwa na kichwa. Itawakatisha tamaa vijana kufanya biashara,” anasema.

Nne, huku mataifa mengi yakiwa hayajaanza kufanya biashara kikamilifu chini ya AfCFTA, Linda anashikilia kuwa "ushuru ni wa juu sana wakati wa kufanya biashara kati ya majukwaa ya biashara ya kikanda. Ni rahisi kufanya biashara ndani ya Afrika Mashariki kuliko na mataifa ya Afrika Magharibi.

Tano, jinamizi la utaratibu wa usafirishaji.

"Huku tukizungumza kuhusu utaratibu wa usafirishajii, usafirishaji ndani ya bara ni mgumu. Kwa wafanyabiashara wengine, ni rahisi na nafuu kuagiza bidhaa kutoka Uchina kuliko kutoka nchi jirani ya Afrika, hata kama ubora wa bidhaa ni sawa.

Mtazamo chanya

Hata hivyo, AfCFTA inalenga haswa kushughulikia wasiwasi wa Linda ambao unaeleza ni kwa nini biashara ya ndani ya Afrika iko katika asilimia 16 tu (16 per cent). Na mtazamo ni chanya zaidi kuliko wa utamaushi.

Kando na kuzinduliwa mnamo Oktoba 2022 kwa Mpango wa Biashara Elekezi, sasa kuna Mifumo ya Malipo ya Mwelekeo-wa-Kiafrika (Pan-African Payment and Settlement Systems),  Africa Trade Observatory na Kitabu cha Ushuru (Tariff Book) .

Mnamo Januari 2023, Kamati ya Kiufundi ya AfCFTA ya Haki na Masuala ya Kisheria ilikamilisha uchakachuaji wa kisheria wa Itifaki za Uwekezaji, Ushindani, na Miliki Bunifu.

Itifaki hizi muhimu zinatarajiwa kuidhinishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia mwishoni mwa Februari 2023.

Hizo lazima habari njema kwa mjasiriamali kijana kama Linda.

“Ni vijana wa Afrika ambao watafanya bara la Afrika kuwa la viwanda kupitia AfCFTA. Na utengenezaji na uongezaji thamani ni viambata muhimu,” anasisitiza.